Uzalishaji wa mazao ya chakula wapaa kwa asilimia 19

Na Lucy Samson
3 May 2024
Mazao ya chakula kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ni pamoja na mahindi, mchele, ngano, mtama, ulezi, uwele, muhogo, maharage, mikunde, ndizi, viazi vitamu na viazi mviringo.
article
  • Wafikia tani milioni 20.4 kwa mwaka wa kilimo 2022/23.
  • Ni fursa kwa Tanzania kunufaika kiuchumi kupitia biashara  ya mazao.

Tanzania imeripoti ongezeko la mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2022/23 jambo litalochochea kuimarika kwa usalama wa chakula nchini pamoja na kukuza biashara ya mazao hayo hatua itayochechemua uchumi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya chakula nchini humo.

Ongezeko hilo la asilimia 19 linakuja wakati ambao maeneo mengine ikiwemo mataifa jirani kama Kenya na Malawi yanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi zilizoathiri mavuno ya msimu wa mwaka 2022/23 na hivyo kutoa nafasi kwa Tanzania kupata soko la mazao hayo.

Mazao ya chakula kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ni pamoja na mahindi, mchele, ngano, mtama, ulezi, uwele, muhogo, maharage, mikunde, ndizi, viazi vitamu na viazi mviringo.

Wizara hiyo imebainisha kuwa jumla ya tani milioni 3.3 zimeongezeka kutoka tani milioni 17.1 zilizozalishwa katika msimu wa kilimo wa mwaka  2021/22 na kufikia tani milioni 20.4 zilizozalishwa mwaka 2022/23. 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliyekuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka 2024/25 aliwaambia wabunge kuwa katika msimu wa mwaka 2022/23 uzalishaji wa mazao ya nafaka ulifikia tani milioni 11.4.

“Katika kipindi hicho, uzalishaji wa mazao ya nafaka ulikuwa tani milioni 11.4 ikilinganishwa na tani milioni 9.2 msimu wa kilimo 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 23.9,” alisema Bashe jijini Dodoma. 

Kwa mujibu wa waziri huyo, uzalishaji wa mazao yasiyo nafaka ulikuwa tani milioni  8.9 ikilinganishwa na tani milioni 7.9 katika msimu wa kilimo 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 13.1.

Uzalishaji huo unafanya utoshelevu wa chakula kwa mwaka 2023/2024 kufikia asilimia 124 ikilinganishwa na lengo la asilimia 150 ifikapo 2030.

Huenda ongezeko hilo la uzalishaji wa chakula ni matokeo ya kupaa kwa bajeti ya kilimo ambapo kwa mwaka 2022/2023 ilifikia Sh751.12 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh268.90 bilioni ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya umwagiliaji ambayo itachochea uzalishaji zaidi wa mazao ya chakula.

Halmashauri 19 zakwamuliwa na wimbi la njaa

Wakati uzalishaji wa mazao ukipaa nchini Tanzania, hali ya chakula haikuwa nzuri katika halmashauri 19 nchini, jambo lililoilazimu Serikali kupitia Wakala wa Chakula wa Serikali (NFRA) kutoa tani 481.9 za chakula cha msaada.

Halmashauri hizo ni pamoja na Muleba iliyopewa tani 23.16, Shinyanga Manispaa (tani 4.776), Kakonko (tani 5.184), Geita DC, Geita Mji na Nyang’hwale (tani 33.4) na Bahi ya mkoani Dodoma ilipata tani 8.1.

Nyingine ni Temeke, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni zote za Dar es Salaam ambapo tani 100 zilitolewa na Halmashauri za Moshi, Hai na Same za mkoani Kilimanjaro zilipewa tani 88.88 pamoja na Halmashauri za Rufiji na Kibiti za mkoani Pwani zilipewa tani 40.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa