Dar es Salaam. Makontena nane ya baridi yanatarajiwa kuanza kusafirisha mboga na matunda kutoka mikoa ya Morogoro na Dodoma kwenda Dar es Salaam kupitia Reli ya Kati kuanzia Oktoba 2026, katika hatua mpya ya kupunguza upotevu mkubwa wa mazao ya bustani unaowakosesha wakulima mapato kila mwaka.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amesema hayo Juni 16, 2026 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Lucy Kombani, aliyetaka kujua mikakati ya kukabiliana na upotevu wa mazao ya mboga na matunda baada ya mavuno.
“Vile vile Serikali inashirikiana na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa Duniani (WFP) kupunguza upotevu wa mazao ya mboga na matunda katika mikoa ya Morogoro na Dodoma kupitia Reli ya Kati…
… Ambapo WFP imetoa kontena nane za baridi kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ajili ya kusafirisha mboga na matunda kutoka mkoa wa Morogoro na Dodoma kuelekea katika masoko mkoani Dar es Salaam,” alisema Silinde.
Mbali na mradi huo, Silinde alieleza kuwa juhudi nyingine zinaendelea kutekelezwa ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa wakulima na maafisa ugani, usambazaji wa miongozo ya usimamizi wa mazao baada ya mavuno pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ili kupunguza hasara zinazotokana na kuharibika kwa mazao kabla hayajafika sokoni.
“Serikali imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kusaidia wakulima kukabiliana na upotevu wa mazao ya mboga na matunda ikiwemo kusambaza miongozo ya usimamizi wa mazao baada ya mavuno,” aliongeza
Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya mazao ya bustani ikiendelea kuwa miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi nchini.
Takwimu za Chama cha Wakulima wa Mazao ya Bustani Tanzania (Taha) zinaonyesha mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya bustani nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 64 hadi zaidi ya dola milioni 779 katika kipindi cha miaka ya karibuni, huku sekta hiyo ikichangia ajira, lishe na ukuaji wa uchumi.
Pamoja na ukuaji huo, upotevu wa mazao baada ya mavuno umeendelea kuwa changamoto kubwa. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 50 hadi 70 ya matunda na mboga zinaweza kuharibika kabla ya kuwafikia walaji kutokana na uhaba wa maghala ya kisasa, miundombinu hafifu ya usafirishaji, ukosefu wa mifumo ya baridi na changamoto za masoko.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuweka mikakati ya kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Mwaka 2018, Wizara ya Kilimo ilizindua Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Mavuno wa mwaka 2018-2027 unaolenga kupunguza upotevu wa mazao ya kilimo, hususan matunda na mboga ambazo hupotea kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko mazao mengine kutokana na kuharibika kwa haraka.
Kwa mujibu wa Silinde, wizara imeandaa na kusambaza miongozo saba ya usimamizi wa mazao ya bustani baada ya mavuno ikihusisha mazao ya vitunguu, nyanya, pilipili hoho, bamia, kabichi, karoti na mboga za majani, huku ikiahidi kuongeza mafunzo na warsha kwa wakulima hususan wa Mkoa wa Morogoro.