Jinsi unavyoweza kukausha majani ya mlonge

Na Fatuma Hussein
4 Dec 2025
Ili kuhakikisha virutubisho hivi vinadumu kwa muda mrefu na katika ubora unaostahili ni muhimu kufuata taratibu madhubuti za kukusanya, kusafisha na kukausha majani haya. 
article
  • Ni pamoja na kuvuna majani kwa mbinu zinazolinda virutubisho na ubora wake.
  • Hatua za kuosha, kuondoa maji ya ziada na kutenganisha majani madogo na vikonyo ni muhimu kuzingatiwa.

Majani ya mlonge ni chanzo muhimu cha virutubisho vya asili vinavyosaidia kuboresha afya na lishe ya binadamu.

Ili kuhakikisha virutubisho hivi vinadumu kwa muda mrefu na katika ubora unaostahili ni muhimu kufuata taratibu madhubuti za kukusanya, kusafisha na kukausha majani haya. 

Baada ya kuelewa kwa kina faida lukuki zinazopatikana katika majani ya mlonge pamoja na njia mbalimbali za kuyatumia katika maisha ya kila siku kupitia makala zilizopita na leo tunasonga mbele kwenye hatua nyingine muhimu ya ukaushaji wa mmea huu.

Kwa mujibu wa Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga, Pendo Majengo anasisitiza kuwa kukausha mmea huu ni njia bora zaidi kwa sababu utakaa kwa muda mrefu na ni njia nzuri na sahihi ya kuutunza.

Kama ilivyo kwa mazao mengine mfano chai, kahawa, mwani na hata zabibu, mlonge pia unahatua zake za kukaushwa na JikoPoint.co.tz tupo kwa ajili ya kukujuza hatua hizi.

Kuvuna

Hatua ya kwanza katika mchakato huu ni kuvuna majani kutoka kwenye miti yenye afya na ambayo majani yake hayajakomaa sana, kwani majani mabichi huwa na virutubisho vingi na ni rahisi kukauka. 

Majengo ameongeza kuwa kuvuna kunapaswa kufanyika wakati wa asubuhi au jioni na kuepuka mvua au hali ya unyevunyevu mkubwa ili kupunguza hatari ya kuoza na kuharibika kwa majani.

Wakati wa kuvuna majani ni muhimu kuchagua majani ambayo hayaharibiwa na wadudu. Picha/Canva.

“Yale matawi unayavuna vizuri, unayachambua, unayatoa kwenye vijiti ili vibaki peke yake, kisha unayaosha kwa maji ya baridi ili kutoa michanga. Wakati wa kuvuna usitumie maji ya moto kwa sababu tunapoteza vitamini C,” anashauri Afisa Lishe Majengo huku akisisitiza kutokutumia maji ya moto kwa ajili ya kuosha majani.

Baada ya kuvuna, majani yanapaswa kuchambuliwa kwa kuondoa matawi makubwa, magome na majani yaliyoathirika na wadudu ili kubakisha majani safi yanayofaa kwa matumizi. 

Zaidi ya hayo, ni muhimu kuvuna kwa mbinu za usafi ambapo unashauriwa kuosha mikono kabla ya kuanza kuvuna majani. 

Kuondoa majani kutoka kwenye matawi

Kwa kuwa virutubisho vingi zaidi hupatikana kwenye majani (leaflets) badala ya vijiti vya majani (petioles), ni vyema kuondoa majani kutoka kwenye matawi kwa ustadi. 

Huenda isiwe rahisi kuondoa kila jani dogo moja moja, lakini jitahidi kuondoa sehemu kubwa ya kikonyo hicho. 

Majani ya mlonge yana wingi wa vitamin C ambayo ni muhimu katika kuimarisha mwili. Picha/ Canva.

Fanya hivyo kwa kuyashika majani na kuyavuta kwa upole, hili linaweza kufanyika kwa kuvuta majani kwa mkono au kutumia mchakato wa kuvuta majani kutoka kwenye matawi ya majani.

Ondoa sehemu zenye nyuzi kwa kutoa majani kutoka kwenye kila tawi dogo la jani. Majani madogo huwa rahisi zaidi kuondoa ikiwa utayatoa mara tu baada ya kuoshwa.

Kusafisha majani 

Majani yanapaswa kuoshwa kwa kuyaweka kwenye bakuli safi au maji safi kisha kuzizungusha kwa upole ili kuondoa vumbi, mchanga na uchafu mwingine.

Ili kuzuia vijidudu, unaweza kutumia kuosha majani hayo kwa kutuma  chumvi kwa dakika tatu hadi tano kabla ya kuosha majani tena kwa maji safi. 

Mara baada ya kuosha, majani yanapaswa kuondolewa maji ya ziada kwa kupiga au kuzungusha kwenye kitambaa safi au kuwekwa kwenye chujio ili maji yachuruzike.

Kukausha majani 

Hatua inayofuata ni ukaushaji wa majani, ambapo majani haya yanapaswa kukaushwa katika maeneo yenye kivuli, mwanga wa kutosha na mzunguko mzuri wa hewa. 

 “Usikaushe majani chini ya jua kali kwa sababu joto la moja kwa moja hivyo ni vyema kuyaanika katika eneo lenye kivuli na mwanga wa kutosha ,” ameeleza Majengo.

Aidha, majani yanapaswa kusambazwa kwa usawa katika trei, chujio au kitambaa safi kilichonyooka na kugeuzwa kila siku ili kuzuia ukungu na kuhakikisha kukauka kwa usawa. 

Ni muhimu kutumia maji ya baridi kuosha majani haya ili kuhifadhi virutubisho vyake. Picha/ Canva.

Pia, Majengo anasisitiza umuhimu wa kutumia vifaa vinavyoweza kuondoa maji yote kwenye majani ili kuhakikisha majani yamekauka kikamilifu na hayana unyevunyevu unaoweza kusababisha kuoza.

Kukausha majani kunachukua siku tatu hadi saba kulingana na hali ya hewa na joto la mazingira.

Kusaga majani yaliyokauka

Kusaga majani ni hatua nyingine ambapo majani yaliokauka yanaweza kusagwa kwa mashine za kusagia mfano blenda au kinu cha asili kwa usafi ili kuepuka uchafu na kupoteza ubora. 

Baada ya kusaga, unga unachujwa kwa kutumia chujio ili kuondoa vipande vikubwa ambavyo havijasagwa vizuri.

Unga wa mlonge wenye ubora hubaki na ladha na harufu ya asili pamoja na virutubisho muhimu.

Kuchanganya viungo na kuhifadhi

Kwa kuongeza ladha na faida za kiafya, unga wa mlonge unaweza kuchanganywa na viungo vya asili kama karafuu, tangawizi na pilipili mtama.

Viungo hivi pia vinapaswa kukaushwa vizuri kabla ya kuchanganywa.

Unga wa mlonge unapaswa kuhifadhiwa katika chombo kisafi, kisichopitisha hewa na kuwekwa katika sehemu kavu na yenye ubaridi ili kuzuia kuoza au kushambuliwa na wadudu.

Kukausha majani ya mlonge kunahitaji ufuatiliaji wa makini wa hatua zote zilizoelezwa hapa ikiwemo mchakato mzuri wa kuvuna, kusafisha, kuondoa majani, kukaushaji, kusaga na kuhifadhi ili kuhakikisha virutubisho vinadumu na kuwa ya ubora wa hali ya juu. 

Kwa mtu yeyote anayetaka kutumia mlonge kwa lishe ya familia au kuanzisha biashara ya bidhaa asilia, kufuata miongozo hii ni msingi wa mafanikio endelevu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa