Unavyoweza kuandaa saladi ya viazi na njegere

Na Lucy Samson
16 Dec 2022
Saladi ni mchanganyiko wa mboga mboga, matunda na viungo vilivyopikwa au vibichi.
article
  • Saladi ni sehemu muhimu ya mlo wa asubuhi, mchana au jioni.
  • Ni chanzo cha vitamini, wanga na protini.
  • Ni rahisi sana kuandaa.

Saladi ni moja kati ya chakula muhimu kwa sababu hupendezesha meza lakini pia huongeza ladha na vitamini mwilini.

Saladi ni mchanganyiko wa mboga mboga, matunda na viungo vilivyopikwa au vibichi vinavyoweza kuliwa vyenyewe au ikasindikiza mlo mwingine wa asubuhi, mchana au jioni.

Msimu huu wa sikukuu ambapo familia husheherekea pamoja, ni vyema kujaribu kitu kipya kitakachonogesha msosi wako.

Kwenye makala haya utajifunza jinsi utakavyoweza kutengeneza saladi ya viazi na njegere ambayo pia ni chanzo cha vitamini, wanga pamoja na protini.

Maandalizi

Hatua ya kwanza ya maandalizi ya saladi yetu inaanza kwenye kumenya viazi na kuviosha.

Baada ya kuosha vikate kate saizi ndogo na uviweke kwenye sufuria kwa ajili ya kuchemsha.

Washa jiko, bandika sufuria yenye viazi ongeza chumvi kiasi na uache vichemke kwa dakika 20.

Wakati unasubiri viazi viive chambua njegere, katakata kitunguu maji, kitunguu cha majani, karoti na hoho.

Baada ya dakika 20 epua viazi vichuje ili kuondoa maji ya moto nanuongeze maji ya baridi au vipandde vya barafu kuzuia viazi visiendelee kuiva na kurojeka.

Bandika njegere kwa dakika 30 au zaidi mpaka utakapohakikisha zimeiva. Zitoe motoni na uweke pembeni. Kwenye bakuli safi anza kuweka vitunguu, karoti na hoho, kisha malizia na njegere na ongeza vijiko kadhaa vya mayonise na uchanganye vizuri.

Baada ya kuchanganya viungo vyote ongeza viazi na uvikoroge kiasi ili vichanganyike na mayonise na viungo vingine.

Ongeza kijiko kimoja cha maji ya limao au ndimu pamoja na chumvi kiasi. Mpaka hapo saladi yako itakuwa tayari kuliwa.

Unaweza kuiweka kwenye jokofu kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa