“Usiniambie tena mambo ya ugali wa nazi.” Hilo ndilo neno ambalo sikuamini ningelisikia kutoka kwa rafiki yangu Invocavity.
Ilikuwa ni Jumapili, moja ya siku ambazo napenda kutumia muda wangu mwingi jikoni kujaribu mapishi tofauti. Siku hiyo nilikuwa nimeamua kupika ugali wa nazi, chakula ambacho huenda hata wewe umeshangaa kukisikia.
Nakumbuka siku hiyo niliamka muda wa saa tano asubuhi. Baada ya kujitupia juba na kanga kubwa ya Kizanzibar nilielekea gengeni kwa mama Dokta kununua mahitaji.
Kwa kuwa nilikuwa peke yangu nilinunua unga wa Sembe nusu niliweka na akiba ikitokea hata mgeni amekuja basi nusu inatosha, kisha nilichukua nazi kubwa mbili, vitunguu maji, samaki wa sato aliyekaangwa, karoti, kitunguu swaumu , pilipili mboga/hoho, nyanya, mchicha na ngogwe/nyanya chungu huyo nikarudi nyumbani na kifurushi changu cha madikodiko.
Kama nilijua, wakati naandaa mahitaji yangu, mara ghafla rafiki yangu Invocavity akaingia jikoni akiwa ameshika tumbo kwa njaa, akanita kwa jina lake la utani kama kawaida ya watu wa Chuga “mama mzuri, unapika nini?”
“Ugali wa nazi,” nikamjibu huku nikiendelea kukuna nazi. Hakumaliza hata sekunde mbili alicheka sana ilibakia kidogo nimfukuze.
“Yaani wakishua mnazingua sana! Ugali wa nazi tena? Hapa ni hasara tupu.”Sikubishana naye. Nilijua sahani ndiyo ingetoa majibu.
Basi katika heka heka zangu za upishi Invocavity akanambia wakati unakuna nazi ngoja nikusaidie kuandaa vitu vingine nikaona fresh tu mwamba kaamua kutoa msaada nikachukua beseni la maji nikamuwekea vitunguu, nyanya, karoti, hoho na kisu kisha nikaendela na kukuna nazi.

Mmmh!! unaweza kujiuliza huyu aliwasha jiko saa ngapi? usijali nilikuwa natumia ‘pressure cooker’ ambazo Jikosokoni.co.tz wanauza kwa bei rahisi na mimi nililipa kidogo kidogo kisha nikachukua baada ya kumaliza.
Wakati rafiki yangu akiendelea kutoa machozi baada ya kukata kitunguu, mimi nilikuwa nakamua tui la nazi kwa ajili ya mchuzi na ugali.
Baada ya kumaliza kuandaa mahitaji yote nilianza kuunga samaki kwa viungo vyote muhimu kisha nikapika mchicha ambao nilitumia karoti na kitunguu, kwa sababu sikutaka uive sana nilitumia dakika saba tu.
Baada ya kutoa mchicha na kusafisha sufuria niliwasha ‘Pressure Cooker’ na kuendelea na mapishi. Nikachanganya tui la nazi nililoandaa na maji kikombe kimoja kwenye sufuria kisha nikaacha vichemke.
Harufu ya nazi ilianza kuenea jikoni na hata Invocavity aliyekuwa anatania akaanza kunitazama kwa macho ya udadisi.
Nilichukua unga kidogo na kukoroga ili kupata uji mzito, na ulipochemka nikaanza kusonga kama ugali wa kawaida unavyosongwa. Siri ya ugali huu ni kutokuharakisha bali kusonga taratibu mpaka uhakikishe kuwa ugali umeiva. Unaweza kutumia dakika 10 hadi 15.
Baada kuhakikisha kuwa ugali umeiva vizuri nilipakua ugali kwenye sahani, wakati huo samaki niliemuandaa tayari alikuwa ananukia mezani.
Nilipomkaribisha Invocavity alianza kula kimya kimya bila kusema chochote.
Dakika chache baadaye nikamuona anamalizia mchuzi uliobaki kwenye sahani kwa kipande cha ugali. Mwishowe akakomba sahani kanakwamba si yeye aliyekuwa akiucheka ugali huu na kuniita wakishua.
Nikamuuliza, “Vipi, bado ni hasara?” Akacheka na kusema, “Sikuwahi kujua ugali wa nazi una ladha hivi. Wiki ijayo ukipika tena usisahau kunialika.”
Tangu siku hiyo Invocavity huwa akinikuta nataka kupika anaanza kunisaidia tu kuandaa viamba upishi wala haulizi tena maswali mengi .
Kama hujawahi kujaribu ugali wa nazi basi jaribu leo uone utamu wake.