Jinsi ya kupika pilau ya nazi tamu kwa sikukuu ya Eid

Na Fatuma Hussein
20 Mar 2026
Pishi hili ni mbadala wa aina nyingine za pilau zilizozoeleka ambazo hupikwa mara kwa mara katika matukio muhimu.
article
  • Pishi hili ni mbadala wa aina nyingine za pilau zilizozoeleka ambazo hupikwa mara kwa mara katika matukio muhimu.

Pilau ni miongoni mwa vyakula maarufu ambavyo hupendelewa kutumiwa katika sherehe, tafrija na sikukuu mbalimbali ikiwemo ya Eid.

Ingawa kuna aina nyingi za pilau, pilau ya nazi inaweza kuwa ya kipekee inayoweza kunogesha sikukuu ya aina yoyote ukilinganisha na aina nyingine za msosi huo ambazo zimezoeleka.

Mbali na harufu nzuri ya nazi inayoongeza thamani ya msosi huu, pilau hilo lina ladha tamu inayoweza kuwavutia walaji, hivyo salia nami mpaka mwisho wa makala hii ujifunze kuiandaa,

Mahitaji

  • Mchele 
  • Tui la Nazi
  • Vitunguu Maji
  • Kitunguu saumu (garlic) na tangawizi.
  • Pilau masala
  • Binzari nyembamba (cumin).
  • Nyama (unaweza kutumia nyama ya ng’ombe au kuku iliyochemshwa (hiari).
  • Chumvi, 
  • mafuta ya kupikia, 
  • karoti kwa ajili ya nakshi.
Pilau la nazi pia linafaa sana kwa baadhi ya walaji ambao wana mzio au ‘alergy’ na nyama.Picha| Jinsi ya kupika/Facebook.

Hatua kwa hatua namna za kupika pishi hili

Anza kwa kuandaa mahitaji yote yatakayotumika yani kuchambua mchele, kukuna na kuchuja nazi kumenya na kutwanga vitunguu swaumu pamoja na kuchemsha kitoweo utakachotumia

Baada ya hapo washa jiko bandika sufuria na ikipata moto weka mafuta ikifuatiwa na vitunguu maji kisha uanze kukaanga. Siri ya pilau kuwa na rangi nzuri ni kuhakikisha unavikaanga vitunguu mpaka viwe na rangi ya kahawia (brown) bila kuungua. Rangi hii ya vitunguu ndiyo itakayohamia kwenye mchele baadaye.

Vitunguu vikishageuka rangi, ongeza tangawizi na kitunguu saumu vilivyosagwa. Kaanga kidogo ili kuondoa harufu mbichi, kisha ongeza pilau masala na binzari nyembamba. 

Kama unatumia nyama, iongeze katika mchanganyiko wako na uikaange kidogo ili ichanganyikane na viungo. Unaweza pia kuongeza supu kidogo ya nyama ili kuimarisha ladha.

Vituu maji hulipa pilau rangi nzuri ya kahawia na ladha tamu. Picha |Dina Marious/Youtube.

Katika sufuria hiyo hiyo ongeza chumvi, tui la nazi pamoja na maji au supu kulingana  na kipimo cha mchele kisha uache ichemke.

Baada ya tui kuanza kuchemka, weka mchele ulioshwa vizuri. Katika hatua hii, unaweza pia kuongeza karoti zilizokwaruzwa ili kuleta muonekano mzuri na harufu ya ziada.

Funika sufuria vizuri na upunguze moto uwe mdogo sana. Acha pilau iive kwa kutumia mvuke kwa takriban dakika 15 mpaka 20. Hii inahakikisha mchele unaiva vizuri bila kupondeka na tui lote linakauka sawasawa.

Pilau yako ya nazi sasa itakuwa tayari, ikiwa na rangi nzuri ya kahawia na mchele wa mmoja mmoja. Inapendekezwa ipakuliwe ikiwa moto ikiambatana na kachumbari safi, pilipili, au ndizi mbivu kwa ajili ya kufurahia zaidi chakula cha Eid pamoja na familia na marafiki.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa