Safari ya kuandaa mkakati wa kitaifa wa nishaji jadidifu yaiva

Na Daniel Samson
18 Nov 2022
Kuundwa na kuanza kutekelezwa kwa mkakati huo kutakua ni hatua muhimu kuongeza matumizi ya nishati jadidifu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. 
article

  • Serikali yasema utatoa mwelekeo sahihi wa matumizi ya nishati hiyo nchini.
  • Baadhi ya wadau wasema iende mbele na kuanzisha sera ya nishati jadidifu. 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na uandaaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidi, wadau wa maendeleo wameishauri Serikali kuwa na sera mahususi ya nishati hiyo itakayoongeza uwajibikaji na kasi ya matumizi ya vyanzo vyake. 

Nishati Jadidifu ni nishati mbadala inayozalisha umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia itokanayo na vyanzo asilia kama vile mwanga wa jua, nguvu ya upepo, kinyesi, maji na joto kutoka ardhini na ni endelevu. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati mkakati wa mkakati wa kitaifa wa nishati jadidi ulianza kuandaliwa Julai 2022 na unatarajia kukamilika Februari 2023.

Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Wizara ya Nishati, Emillian Nyanda amesema zoezi la kutengeneza mkakati huo linashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa nishati jadidifu ili kupata mawazo ya pamoja yenye maslahi kwa Taifa. 

“Mkakati huu utakuwa ni nyenzo muhimu ya kuongeza matumizi ya nishati jadidifu ambayo Serikali inaipa umuhimu wakati huu,” amesema Nyanda aliyekuwa akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika warsha ya waandishi wa habari iliyoandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi ya Mazingira (Tatedo). 

Warsha hiyo ililenga kuongeza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa nishati jadidifu na namna wanavyoweza kuwa mabalozi wa nishati hiyo safi na salama kwa jamii.

Kuundwa na kuanza kutekelezwa kwa mkakati huo kutakua ni hatua muhimu kuongeza matumizi ya nishati jadidifu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. 

Mpango Mkakati wa Uzalishaji wa Umeme wa mwaka 2016 (The Power System Master Plan 2016) uliotolewa na Wizara ya Nishati unaonyesha kuwa umeme unaozalishwa na vyanzo vya upepo, jua na jotoridi unachangia megawati 3.8 tu kwenye gridi ya Taifa yenye megawati zaidi ya 1,601. 

Nishati safi inaweza kuwakomboa wanawake kutoka kwenye umaskini na magonjwa mbalimbali na kuwawezesha kuboresha maisha yao kiuchumi. Picha | Tatedo.

Maeneo yatakayozingatiwa katika mpango huo

Kwa mujibu wa andiko la uchambuzi kuhusu msaada wa kitaalam kwa ajili ya Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu uliotolewa na Wizara ya Nishati na Jukwaa la Mabadiliko ya Tabianchi (Forum CC), mkakati huo utajikita katika maeneo makuu matano ya kimkakati ikiwemo ujumuishaji wa rasirimali zitakazotumika kutekeleza mkakati huo. 

Maeneo mengine ni kuhimiza matumizi ya nishati jadidifu, fursa za teknolojia zinazopatikana kwenye nishati na kuunda mifumo ya kitaasisi itakayofanya kazi kwa pamoja. 

“Mkakati utahakikisha unatambua athari chanya za usalama wa nishati na kufungua fursa za kukuza na kutangaza teknolojia za nishati jadidifu,” inaeleza sehemu ya andiko hilo. 

Msingi na utambuzi wa maeneo hayo ya kimkakati umetokana na sera, mipango, changamoto na pengo la sasa lililopo katika sekta ya nishati jadidifu ili kuhakikisha inapewa msukumo wa aina yake wakati wa utekelezaji. 

Mpango wa Taifa wa Nishati Jadidifu siyo tu utarahisisha upatikanaji wa nishati jadidifu lakini ni chombo muhimu cha utekezaji wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa nishati endelevu kwa wote (SEAforALL) ambao Tanzania inautekeleza.

SEforALL inalenga kuwafikishia nishati watu wote, kuongeza ufanisi na ubora wa nishati mchanganyiko duniani. 

Ili kuwezesha jamii kujitegemeza kifedha, kampuni ya Vodacom Tanzania inashirikiana na wadau wa nishati jadidifu
kuwajengea uwezo wananchi kutengeneza jiko banifu la kuoka mikate. Jiko hili rafiki wa mazingira litawawezesha kujiongezea kipato. Picha | Vodacom Tanzania.

Hata wakati Serikali ikiendelea na uundaji wa mkakati huo, baadhi ya wadau wameshauri kuwa Serikali ingetunga sera mahususi ya nishati jadidifu kuliko kuwa na mikakati ambayo inaweza isiwe na matokeo makubwa.

Meneja Nishati wa Tatedo, Mary Swai amesema kwa sasa matumizi ya nishati jadidifu hayaepukiki na ili kuwe na msukumo wa kweli kuhusu matumizi yake, utungwaji wa sera ni muhimu. 

Swai amesema ni kweli Serikali ina Sera ya nishati lakini nishati jadidifu ni suala la pana linahitaji msukumo wake kwa sababu inatoa suluhu endelevu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inakabiliana nayo kwa sasa.

Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inaitambua nishati jadidifu kama sekta muhimu inayoweza kuchangia maendeleo ya nishati nchini Tanzania kwa kurahisisha upatikanaji na matumizi yake. 

Naye Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Tatedo, Shima Sago amesema ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati jadidifu hasa kwa shughuli za kupikia, elimu itolewe zaidi kwa wananchi ili wafaidike na faida zake. 

“Tanzania tuna vyanzo vingi vya nishati jadidifu ambavyo tukivitumia vizuri vitasaidia kupunguza ukataji wa miti,” amesema Sago katika warsha hiyo. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa