Viazi vyekundu, vinavyojulikana kitaalamu kama beetroot ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho muhimu sana kwa mwili.
Ingawa mara nyingi hutumiwa kama mboga ya kawaida jikoni ikiwa imechemshwa, kukaangwa au kuchomwa viazi hivi pia hutengeneza juisi tamu na yenye faida nyingi.
Watu wengi hupendelea kuchanganya juisi ya beetroot na karoti, tangawizi au tufaa ili kuongeza ladha na virutubisho.
Viazi hivi hutambulika zaidi kwa rangi yake nyekundu, ingawa baadhi ya aina zake zinaweza kuwa za njano au nyeupe.
Kama ulikwa bado hujajua kwanini utumie viazi vyekundu basi makala hii ipo kwa ajili ya kukujuza faida za kutumia viazi hivi.
Viazi vyekundu vina ānitratesā zinazosaidia kupanua mishipa ya damu, kupunguza msongamano na kuboresha mtiririko wa damu.
Hii hupunguza mzigo kwa moyo na hatari ya kiharusi.
Tovuti ya masuala ya afya ya healthline, inaeleza kuwa matumizi ya viazi hivi husaidia kuimarisha afya ya mwili ikiwemo kushusha shinikizo la damu mwilini, kusaidia mishipa ya damu kupanuka na hivyo kupunguza presha ya damu, na huweza kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi.
Beetroot imeonyeshwa kushusha shinikizo la damu kutokana na nitrates zinazogeuzwa kuwa ānitric oxideā, ambayo hupanua mishipa.
Healthline inathibitisha kuwa ulaji wa beetroot hupunguza presha na hatari ya magonjwa ya moyo.

Tafiti pia, kama ile ya Leah T. Coles na Peter M. Clifton (2012), zilionyesha kupungua kwa 4ā5 mmHg baada ya watu kunywa juisi ya beetroot.
Na kwa upande wa jarida la The Journal of Nutrition liliongeza ushahidi kuwa wagonjwa wenye presha ya juu waliona upungufu wa 10.8 mmHg baada ya siku 60 wakitumia juisi ya beetroot yenye nitrates.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkoa wa Ruvuma, beetroot/ viazi vyekundu ni mmea wenye uwezo wa kusaidia wagonjwa wa upungufu wa damu,kisukari,kansa na figo.
Uwepo wa madini chuma na folate kwenye viazi vyekundu husaidia kutengeneza chembe nyekundu za damu, ambazo husaidia kupambana na upungufu wa damu.
Frola Mgangala mtaalamu kutoka Kampuni ya Mbegu ya Kiafrika (SeedCo), anasema ābeetrootā āhuongeza wingi wa damu ndani ya saa 24ā na kusaidia wagonjwa wa anemia, wajawazito na watoto.ā
Naye, Mtaalam wa Afya kutoka zahanati ya Shaprema iliyoko mkoani Geita Fredrick Pastory, katika mahojiano na JikoPoint ameeleza kuwa, viazi vyekundu ni muhimu kwa kuwa vina madini yanayosaidia kuongeza damu mwilini.
āViazi vyekundu utapata ndani yake kuna madini chuma ambayo ni sehemu ya utengenezaji wa damu, pia inakuwa imebeba vitamini B9 ambayo inasaidia kwenye uzalishaji wa chembe hai nyekundu za damu,ā ameeleza Pastory.

Antioxidants na betalains kwenye beetroot husaidia kupunguza radikali huru ambazo zinaweza kuharibu seli na kuongeza hatari ya saratani.
Pastory ameeleza kuwa radikali huru zikizidi mwilini zinachochea saratani, na beetroot husaidia kupunguza hatari hiyo kwa kupunguza mkusanyiko wa radikali huru.
ā Kwenye mwili kuna radikali huru ambazo zinazalishwa zinavokuwa zimerundikana kwa wingi ndani ya mwili vinaweza kupelekea mtu akapata kansa,ā amesema Pastory.
Nitrates kwenye beetroot huongeza mtiririko wa damu sehemu za ubongo zinazohusika na kumbukumbu na uelewa.
Utafiti ulofanywa na jarida la Cleveland Clinic ulibaini kuwa viazi vyekundu vinasaidia kuimarisha afya ya ubongo na mzunguko wa damu kwenye ubongo kutokana na uwepo wa nitrate ambao pia husaidia kazi ya akili na kumbukumbu.

Beetroot ina vitamini A, B6, C, folate, na potasiamu ambazo husaidia utengenezaji mzuri wa homoni na afya ya uzazi.
Pastory pia amesema uwepo wa madini na vitamini vinavyosaidia kuimarisha afya ya mwili kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi kwa sababu virutubisho hivi huchochea uboreshaji wa seli na mzunguko wa damu.
Ni uamuzi mzuri kuimarisha afya yako kwa kutumia viazi vyekundu hata kama hujaambiwa na daktari kwani ni rahisi kupatikana na hukufanya kuwa na kinga imara zaidi katika mwili wako.